Saturday, October 4, 2014

KILAINI! SITTA ANA MSONGO WA MAWAZO KITAIFA.

Posted by Unknown  |  Tagged as:


Dodoma. Sasa ni wazi kwamba Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta ameingia katika mgogoro na viongozi wa dini.

Wakati jana Sitta akirejea kauli yake aliyoitoa hivi karibuni kwamba waraka uliotolewa na viongozi wa Jukwaa la Wakristo Tanzania kuhusu mchakato wa Katiba kwamba "hauna utukufu wa Mungu na wa kipuuzi", viongozi hao wamesema mwanasiasa huyo ahurumiwe kwa kuwa "ana msongo wa mawazo".

Kauli ya Sitta

Sitta alisema nia ya baadhi ya viongozi hao wa dini ni kuliingiza Taifa katika machafuko, jambo ambalo alisema kama mtu mzima na mzee, hatalivumilia.

Waraka huo ulitolewa kwa pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (FPCT) na Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA).

Sitta alilieleza Bunge hilo kuwa lugha iliyotumika kuandika waraka huo aliokuwa nao na kusoma baadhi ya vipengele vyake, haina staha na haifai hata kidogo kutolewa na watu ambao wanahubiri dini na amani.

"Moja ya vitu ambavyo watu wanatakiwa kuviona, hivi wanaposema kuwa rais asimamishe mchakato wa Katiba, wanakuwa na maana gani? Hivi ni Ukristo huo kweli unaotokana na utukufu wa Mungu?" alihoji Sitta huku akishangiliwa na wajumbe. Alikwenda mbali akiifananisha lugha iliyotumika kuandaa waraka huo na ile aliyozoea kuisikia kutoka kwa wajumbe wa Bunge la Katiba wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Akinukuu sehemu ya waraka huo iliyosema "mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba afanye kazi bila ya ubabe," alisema huo ni uongo kwani anafanya kazi kwa weledi mkubwa.

"Jamani, mimi ni Mkristo na wala sina ubabe wala kiburi. Hivi hawa wanaotutukana kule nje hawawaoni? maneno mangapi yanasemwa juu yetu na watu wale, hivi hii siyo siasa jamani? Waraka huo wa maaskofu umesomwa kila mahali na makanisani, unawezaje kusema Rais aifufue Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakati tayari tume hiyo ilishajifufua yenyewe kwa kujibizana na Bunge kila wakati?"

Sitta aliendelea kueleza kuwa akiwa mzee na mtu mzima, atasimamia jambo hilo ,wanzo mwisho.


SOURCE: MWANANCHI.

0 comments:

Popular Posts

Author

Yohana Mwila

Translator

Subscribe to our Mailing List

We'll never share your Email address.
Copyright © 2013 CORRECT NEWSTZ BLOG. Powered by Blogger.
Blogger Template by Bloggertheme9
+255 (784) 033-443yohanamwila@gmail.com