Monday, January 4, 2016

NATOA HOJA : WANAMICHEZO TUJITATHMINI MWAKA 2016 UMEANZA

Posted by Unknown  |  Tagged as:

Kama ilivyo miaka yote, Tanzania imekuwa ikivurunda katika michezo huku vikitolewa visingizio vya kila aina.

Mwaka wa 2015, kimsingi ndiyo umemalizika na ninaweza kusema hakukuwa na mafanikio katika michezo kwa ujumla wake.

Tanzania ilikuwa ikisifika katika fani mbalimbali za michezo, lakini kadri miaka inavyokwenda, imekuwa ikipoteza mwelekeo wake na hata kutia aibu.

Wanamichezo wetu walionyesha hawawezi, wameonyesha bado hawajakomaa mbele ya wanamichezo wa mataifa wenzao ya Afrika na dunia.

Hakika mwaka 2015 ulikuwa wa aibu katika michezo. Tulishindwa kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali hata ya Kanda za Tano, Kanda ya Sita kwa mpira wa kikapu, mikono michuano mbalimbali na mingine mingi ambayo tumeandaa sisi wenyewe.


Inasikitisha kwa kweli kuwa Tanzania imefutika katika ramani ya michezo na kuna kila sababu kuona mwaka huu inarudi upya kabisa.

Ifike hatua kuwe na mfululizo wa kumkabidhi Rais vikombe kwa vijana wake kuwa walichokifanya ndicho hiki.

Hebu, tujiulize, mwaka jana tumemkabidhi Rais vikombe vingapi kuwa vijana wetu wamefanya kazi nzuri nje na ndani ya nchi zaidi ya Azam na Kombe la Cecafa?


Tujiulize, tumemkabidhi medali ngapi Rais kuwa vijana wake wamepigana nje ya nchi na wakaleta heshima? Ni aibu, halafu eti Waziri mwenye dhamana ya michezo, anajisifu kuwa eneo la michezo limepiga hatua?


Kwa mwaka 2016, kuna haja ya kuwa na uwajibikaji wa jumla, vyama vya michezo, Baraza la Michezo la Taifa, BMT, Kurugenzi ya Michezo, wizara kwa ujumla wake kuwa karibu na utendaji wa vyama vya michezo na wadau wa michezo kuona hatua nyingine mpya za mwaka huu.

Nimekuwa nikiandika, hivi BMT wanafanya nini? Hivi na wao watajigamba wanasimamia michezo wakati iko katika hali mbaya? Kurugenzi ya Michezo nayo itasema wanasimamia michezo Tanzania ikiwa katika hali hiyo?


Ni kukumbushana na ninaamini BMT ina kalenda za vyama vyote vya michezo ya mwaka mzima, hivyo ni wajibu wake kuvikumbusha ama kufuatilia kwa karibu maandalizi yake tena kuanzia Januari hii.

Kusiwe na visingizio tena, kwamba kila mmoja anatakiwa kufanya kile anachostahili kufanya ili Tanzania kupiga hatua za mbali katika michezo.

Mafanikio ama kufanya vizuri kwa vyama vya michezo, kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuleta matumaini ya kufanya vizuri katika michezo kimataifa, lakini kama viongozi wataendelea kupigwa ‘AC’ ofisini na viti vya matairi na kuzunguka, kamwe hakutakuwa na maendeleo, hilo liko wazi.

Kuendelea kukimbia pekupeku, mabondia kukosa maandalizi ya maana ni wazi hatuwezi kupata medali.

Hapa yanayofanyika ni masihara tu kwani hata hayo maandalizi ya Michezo ya Olimpiki mwaka huu huko Rio de Janeiro, Brazil maandalizi yake hayaeleweki.

Labda niseme, michezo imepata Waziri anayeweza kwenda na kasi ya sasa, Hapa Kazi tu na ifike hatua mwaka huu uwe wa mafanikio katika michezo kwa kuonyesha dira mpya, mwelekeo mpya na kila mwenye wajibu na majukumu katika michezo, afanye kazi kwa nafasi yake kwa wakati wake.

Ukweli wa Watanzania wanapenda michezo na wako tayari kulipa fedha nyingi kupata burudani, tatizo hao waliopewa dhamana kusimamia sekta ya michezo nchini, wamejaaliwa kwa ubabaishaji wa hali ya juu.

0 comments:

Popular Posts

Author

Yohana Mwila

Translator

Subscribe to our Mailing List

We'll never share your Email address.
Copyright © 2013 CORRECT NEWSTZ BLOG. Powered by Blogger.
Blogger Template by Bloggertheme9
+255 (784) 033-443yohanamwila@gmail.com