Friday, February 7, 2014

BUNGE LA KATIBA NDILO LINALOWEZA KUZIMA HOJA YA SERIKALI TATU.

Posted by Unknown  |  Tagged as:

CCM yapanga mikakati minne kuzima azma hiyo
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeweka mikakati minne mikubwa kuhakikisha kinazima mapendekezo ya serikali tatu ili kubaki na mfumo wa serikali mbili ulioboreshwa, Tanzania Daima Jumatano limebaini.


Msimamo huo wa serikali mbili umekolezwa zaidi juzi na hotuba ya mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, wakati akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa kwa CCM.

 Kikwete alisema sera ya CCM ni serikali mbili na akarejea kauli aliyopata kuitoa wakati wa hotuba yake ya kufunga mwaka kwamba mchakato wa katiba mpya ukivurugika, serikali itarudi kwenye katiba ya sasa ambayo imekuwa ikilalamikiwa kwa miaka yote.


Duru za siasa zinasema kuwa majina ya wajumbe kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) yamekuwa magumu, kwani hayawezi kushawishika kukubaliana na sera ya CCM ya serikali mbili.
Kwa mujibu wa habari hizo, mkakati wa pili ni kupitia kikao maalumu cha Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM.

Habari zinasema kuwa kikao cha NEC kinatarajiwa kukutana siku chache kabla ya Bunge la Katiba ili kutoa msimamo wa chama kuhusu umuhimu wa serikali mbili na ubaya wa serikali tatu.

Kikao hicho ambacho ni mkakati wa pili, kinafuatiwa na mkakati wa tatu wa kuitisha kikao cha wabunge wote pamoja na wale wa Bunge Maalumu kuwaelezea namna ya kuzima mapendekezo ya serikali tatu.
Kikao hicho kitashirikisha wabunge wote, wabunge wa Bunge la Katiba kutoka nje ya Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi.

Habari zaidi zinasema kuwa mkakati wa nne upo kupitia kanuni za Bunge jipya la Katiba.

Inaelezwa kuwa upitishaji wa kanuni hizo utazingatia wingi wa kura za wabunge ambao unatoa nafasi kubwa kwa wabunge wa CCM kupitisha kanuni zitakazowasaidia kuzima hoja ya serikali tatu.

Duru za siasa ndani ya chama hicho tawala zinasema kuwa CCM haiko tayari kwa mfumo wa serikali tatu, kwani inaamini utavunja Muungano.


Mzozo wa muundo wa serikali tatu ulianza baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, chini ya Jaji Joseph Warioba, kuja na rasimu ya kwanza ambapo wananchi wengi walipendekeza mfumo wa serikali tatu.
Baada ya rasimu hiyo, CCM ilipitisha azimio na kulisambaza mikoani hadi ngazi ya chini na kuagiza mabaraza ya katiba yahakikishe yanatoa mapendekezo ya serikali mbili.

Pamoja na njama za CCM kutaka kuchakachua mapendekezo hayo, bado rasimu ya pili ya katiba iliyowasilishwa kwa Rais Kikwete hivi karibuni, imekuja na mapendekezo ya serikali tatu, kinyume cha matarajio ya CCM.

Kutokana na hali hiyo, CCM inaamini sehemu pekee ya kubadilisha mapendekezo hayo ni kwenye Bunge la Katiba ambalo linatarajiwa kukutana wakati wowote mwezi huu.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2013, Bunge Maalumu la Katiba litakuwa na jumla ya wajumbe 635.


0 comments:

Popular Posts

Author

Yohana Mwila

Translator

Subscribe to our Mailing List

We'll never share your Email address.
Copyright © 2013 CORRECT NEWSTZ BLOG. Powered by Blogger.
Blogger Template by Bloggertheme9
+255 (784) 033-443yohanamwila@gmail.com